Wananchi wa Msumbiji wanaoishi mkoani Mtwara, wameshiriki zoezi la upigaji kura la uchaguzi mkuu unaofanyika nchini Msumbiji leo Oktoba 9, mwaka huu.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanamozambiki wanaoishi mkoani Mtwara, Raphael Kamuti amesema mkoa wa Mtwara una zaidi ya vituo Kumi na Sita vya kupigia kura.
Kamuti amesema uchaguzi huo katika vituo vyote vya mkoa wa Mtwara, unaendelea kufanyika kwa amani na hakuna changamoto yoyote iliyojitokeza na watu bado wanaendelea kujitokeza kwa wingi kupiga kura, huku zoezi linatazamiwa kukamilika saa kumi na mbili jioni.
Ametaja baadhi ya vituo hivyo kuwa ni pamoja na Mangaka A na Mangaka B, Msumbiji ya leo, Mtokola, Muungano, Nangomba 1 na Nangomba 2, Maratani, Mnanje , Mkwajuni na Mtawatawa katika wilaya ya Nanyumbu.
Vituo vingine ni Mkanaledi na Likonde vilivyopo manispaa ya Mtwara Mikindani pamoja na kituo cha Madimba kilichopo halmashauri wilaya ya Mtwara.
Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya wanamozambiki wanaoishi mkoani Mtwara Raphael Kamuti amesema huu ni uchaguzi wa nne wao kushiriki wakiwa mkoani humo ambapo uchaguzi wa kwanza walifanya mwaka 2009, wa pili mwaka 2014, uchaguzi wa tatu mwaka 2019 na uchaguzi wa nne ni huu wa mwaka huu wa 2024.