Back to top

MWALIMU MATATANI KUFANYA MAPENZI NA MWANAFUNZI

10 October 2024
Share

Mwalimu Subiri Andson (37) wa Shule Sekondari Nguno iliyoko katika Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya hiyo kujibu tuhuma inayomkabili ya kukutwa akifanya mapenzi na mwanafunzi (17) nyumbani kwake.

Mbele ya Hakimu mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Robert Kaanwa, Mwalimu huyo amesomewa kosa lake moja na Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ya wilaya hiyo, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi  Jaston Mhule.

Mwendesha Mashtaka huyo ameieleza Mahakama kuwa Mwalimu huyo alitenda kosa hilo, kinyume na kifungu cha 130(1)(2)e na 131(1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Akitoa maelezo ya kosa hilo, Mhule ameeleza kuwa katika moja ya Kijiji (jina linahifadhiwa) maeneo ya Sekondari, anakofundisha ndani ya wilaya hiyo, mshtakiwa alimbaka mhanga mwanafunzi wa sekondari mwenye umri wa miaka 17 kwa kufanya nae mapenzi.

Amesema kuwa mnao Oktoba 07, 2024 mshtakiwa aliwekwa chini ya ulinzi wa wananchi baada ya kukamatwa akiwa na mhanga chumbani kwake majira ya saa moja usiku na baada ya kumkamata walimfikisha kituo cha Polisi Itilima.

Baada ya kusomewa maelezo ya kosa hilo, Mshtakiwa alikana, ambapo upande wa mashtaka uliwasilisha shahidi mmoja na kusikilizwa huku mshtakiwa akipelekwa mahabusu baada ya kukosa dhamana.

Hakimu Robert Kaanwa, ameahirisha kesi hiyo mpaka Oktoba 15, 2024 ambapo kesi hiyo itafikishwa mahakamani hapo tena kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa.