Mwenyekitiwa Jumuiya ya Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Taifa (UWT), Mary Chatanda amesema Jumuiya hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia mkakati uliopo wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Chatanda ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akihamasisha wananchi kuachana na matumizi ya nishati isiyo safi na kuanza kupika kisasa kupitia nishati safi ya kupikia.
"Nishati safi ya kupikia upatikanaji wake hivi sasa umekuwa rahisi, pamoja na kuiunga mkono Serikali kwenye ajenda hii, tutaendelea kuishauri kupunguza zaidi gharama za mitungi ya gesi ili wananchi wengi waweze kuimudu." Amesema Chatanda
Ameeleza kuwa, utafutaji wa nishati isiyo safi ya kupikia umekuwa hatarishi kwa wanawake kipindi wanapokuwa maporini wakitafuta kuni kwani wa nakutana na ukatili wa kijinsia na hata katika nyakati wanapochelewa kurejea majumbani.
Amesema nishati safi ya kupikia itawakomboa wanawake na watoto na athari mbalimbali ikiwemo za kiafya na ukatili waliokuwa wakikutana nao wakati wa utafutaji wa kuni.
Tanzania imeanza kutekeleza Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao unaelekeza asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.