Back to top

SHERIA BORA KURAHISISHA USIMAMIZI VYAMA VYA USHIRIKA

13 October 2024
Share

Viwango sawa vya utendaji na utoaji wa huduma za Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo, vimetajwa kuwa chachu ya kuimarisha usimamizi na upimaji wa Vyama hivyo katika maeneo mbalimbali Kimataifa.

Hayo yamebainishwa na Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege wakati akiwasilisha mada kwenye Mkutano wa 24 wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo Barani Afrika, Jijini Naivasha, Nchini Kenya.

Mrajis amesema kuwa utendaji wa vyama hivyo, unapowekewa viwango sawa itasaidia kutathmini utendaji wake baina ya nchi moja na nyingine kwa urahisi na kulinganisha ufanisi wa chama husika.

 Mrajis amebainisha masuala ya ulinganifu wa uandaaji wa Taarifa za kiutendaji za SACCOS katika mataifa yanayoandaa taarifa hizo akitolea mfano Tanzania na Kenya, ukusanyaji wa taarifa husika pamoja na utoaji wa taarifa hizo kwa Umma kumeendelea kuongeza hamasa kwa wananchi kufahamu hali ya utendaji na uendeshaji wa SACCOS katika mataifa husika. Licha ya uwepo wa utofauti wa mazingira na mifumo ya usimamizi katika mataifa.

Aidha, Mrajis aliendelea kusisitiza kuwa licha ya Wanaushirika wa Akiba na Mikopo katika Mataifa mbalimbali kufanya kazi katika mazingira tofauti, bado kuna haja ya Baraza la SACCOS Barani Africa (ACCOSCA) kuandaa Viwango ambavyo vinaweza kutumika katika mataifa mbalimbali kama sehemu ya kupima uendelevu wa SACCOS kwa Taifa moja na Taifa lingine.

Sambamba na kuwasilishwa kwa Mada hiyo, Mrajis pamoja na Watendaji wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania walipata fursa ya kutembelea na  kujifunza masuala mbalimbali katika mabanda ya Maonesho yaliyokuwepo katika Mkutano huo ambapo pamoja na mambo mengine wamejifunza kuhusu muundo na uendeshaji wa Benki ya Ushirika ya Kenya pamoja na bidhaa na huduma zinazotolewa na SACCOS za Kenya.

Aidha, wanaushirika walioshiriki katika kongamano hilo walipata fursa ya kwenda kupanda miti katika maeneo mbalimbali jijini Naivasha kwa lengo la kutunza mazingira. 

Mkutano huo umehudhuriwa na mataifa yapatayo 42 na washiriki zaidi ya 2,000 wamehudhuria kutoka mataifa mbalimbali.  Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania imeambatana na Wanushirika 71 kutoka SACCOS mbalimbali nchini.