Back to top

AFANDE HAJATOKEA TENA, KESI YAAHIRISHWA!

15 October 2024
Share

Kesi ya jinai ya kutuma kubaka na kumuingilia kinyume na maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam inayomhusu Afisa wa Jeshi la Polisi Fatma Kigondo ‘Afande’ imetolewa maamuzi madogo baada ya upande wa mlalamikaji kuiomba mahakama itoe amri ya kukamatwa kwa mtuhumiwa na kufikishwa mahakamani hapo kutokana na mtuhumiwa kutofika tena mahakamani hapo. 

Hakimu anayesikiliza kesi hiyo namba 23627 ya mwaka 2024, Nyamburi Tungaraja wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dodoma, ametoa uamuzi kuwa sio kazi ya mahakama kumkamata mtuhumiwa na kumpeleka mahakamani.

Akizungumza nje ya mahakama hiyo, wakili upande wa mlalamikaji, Peter Madeleka amesema amekusudia kupeleka maombi katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma kuweza kuangalia na kupitia uendeshaji wa shauri hilo kwa kudai ni ukiukwaji wa sheria.

Aidha, wakili Madeleka amebainisha kuwa, amekusudia kumpeleka mahakamani Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma Nyamburi Tungaraja kwa kumkosea heshima mbele ya mahakama baada ya kitendo cha kumfokea.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 16, mwaka huu itakaposikilizwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dodoma.