Naibu Rais Rugathi Gachagua atafika mbele ya Bunge la Senate kesho kujitetea, baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali ombi lake la kumzuia kufika mbele ya bunge hilo.
Hoja ya kumwondoa afisini Gachagua itaendelea kujadiliwa katika Bunge la Seneti ilivyoratibiwa Jumatano na Alhamisi.
Gachagua alitaka mahakama izuie Bunge la Senate kusikiliza kesi yake kwa madai kuwa haki zake za kikatiba zilikiukwa.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Milimani jijini Nairobi, Chacha Mwita kwenye uamuzi wake leo Jumanne alasiri, amesema Senate iko huru kusikiliza na kubaini hatma ya kesi dhidi ya Gachagua.
Wiki iliyopita Bunge la Kitaifa lilipiga kura ya kumng’atua ofisini Naibu Rais kwa kukiuka sheria. Wabunge 281 wakipiga kura ya kumwondoa ofisini huku 44 wakipiga kura ya kupinga hoja hiyo.
Awali, Spika wa Seneti, Amason Kingi, alitangaza kwamba bunge haliwezi kuwekewa vizingiti, na hivyo hoja ya kumwondoa Gachagua mamlakani itaendelea kama ilivyopangwa.
Takriban kesi 29 zimewasilishwa katika mahakama mbalimbali kutaka kuzuia suala la kumwondoa madarakani Gachagua.
Tayari Jaji Mkuu Martha Koome ameunda jopo la majaji watatu kusikiliza na kuamua kesi zinazopinga shughuli ya kumwondoa Gachagua.
Jopo hilo linahusisha majaji Eric Ogola, Anthony Mrima na Freda Mugambi. Bunge la kitaifa wiki iliyopita lilipitisha hoja ya kumng’oa mamlakani naibu rais.