Back to top

HALMASHAURI MKIPIMA VIWANJA ‘ROAD RESERVE’ HATULIPI FIDIA - BASHUNGWA

20 October 2024
Share

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amesema kuwa Serikali haitalipa fidia kwa wananchi ambao wamepimiwa viwanja na  Halmashauri katika maeneo ya Hifadhi za Barabara, zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria kwa ajili ya kuendeleza ujenzi na upanuzi wa miundombinu ya barabara katika maeneo husika.

Bashungwa ametoa kauli hiyo Wilayani Kyerwa, wakati akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, Innocent Bilakatwe, ikiwemo suala la fidia kwa wananchi waliopimiwa maeneo yao na Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa katika Hifadhi ya Barabara.

“Jambo la fidia eneo hili naomba niseme ukweli Halmashauri mlijichanganya mkapima eneo la road reserve, road reserve zipo kwa mujibu wa sheria, kwa hiyo waliojichanganya wakapima na kugawa viwanja watafute namna ya kufanya ila Sisi tunasimamia sheria na tumetenga maeneo hayo kwa ajili ya kujenga barabara”, amesisitiza Bashungwa.

Bashungwa amesisitiza kuwa maeneo yote yaliyotengwa kama hifadhi ya barabara hayaruhusiwi kuendelezwa na wananchi kwa kuwa yanahitajika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara siku za mbeleni.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, Innocent Bilakatwe ameiomba timu ya Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS) kufika katika maeneo hayo ambayo yamepimwa na kuendelezwa na wananchi ili kuweza kutatua suala hilo.