Back to top

DEREVA AJALI ILIYOUA 9 APANDISHWA KIZIMBANI

30 October 2024
Share

#HABARI: Dereva wa basi Shedrack Swai (37) aliyesababisha ajali Oktoba 22.2024 eneo la Ukiligulu, wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza amepandishwa kizimbani jana Oktoba 29,2025 katika Mahakama ya Wilaya ya Misungwi na kusomewa shtaka la kuendesha gari kwa uzembe katika Barabara ya Umma lenye makosa 64 yakiwemo ya kusababisha vifo, majeruhi, uharibifu wa miundombinu na mali.

Akisoma shtaka katika kesi ya Trafiki namba 30855/2024, linalomkabili dereva huyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Misungwi, Esther Marick, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Ramson Salehe akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Lilian Meli alisema mshtakiwa alitenda makosa hayo kinyume na Kifungu cha 41, 63 (2) (b) na 27 (1) cha Sheria ya Usalama Barabarani namba 168 marejeo ya mwaka 2002.

Salehe aliieleza mahakama hiyo kuwa mshakiwa anashtakiwa kwa makosa 64 yakiwemo ya kuendesha gari kwa uzembe katika barabara ya umma  na kusababisha vifo vya watu tisa, kujeruhi 54 na kusababisha uharibifu wa mali pamoja na miundombinu.

“Mshtakiwa (Shedrack Swayi) siku ya Oktoba 22,2024, ukiwa dereva wa gari lanye namba za usajiri T. 458 DYD aina ya Yutong basi uliendesha gari hilo kwa uzembe katika barabara ya umma Mwanza-Shinyanga eneo la Kijiji cha Ukiriguru wilayani Misungwi ambapo ulilipita gari lingine bila kuchukua tahadhari na matokeo yake ukaligonga gari lingine lenye namba za usajiri T. 281 EFG aina ya You tong basi  na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali,” alisema Salehe 

Baada ya kumsomea makosa hayo, mshtakiwa Shedrack Swayi alikiri kutenda makosa hayo yote 64 huku Wakili wa Serikali Mwandamizi Lilian Meli akiiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali (PH).