Rais wa zamani Donald Trump kutoka chama cha Republican, anakabiliana na Makamu wa Rais Kamala Harris katika uchaguzi wa rais wa Marekani leo Novemba 5, unaoshuhudiwa kuwa na ushindani mkali.
Kamala Harris, mwenye umri wa miaka 60, alishinda uteuzi wa Chama cha Democratic, baada ya Joe Biden, kusitisha kampeni yake, na hivyo kuwapa Wademokrat nafasi ya kuwasilisha maono mapya ya Marekani tofauti na ajenda ya Trump.
Harris, Seneta wa zamani, Mwanasheria mkuu wa California, na Mwendesha mashtaka wa San Francisco, aliandika historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza na mtu mwenye asili ya kigeni kuhudumu kama Makamu wa Rais, ikiwa atachaguliwa, atakuwa rais wa kwanza mwanamke, katika historia ya Marekani.
Uchunguzi unamuonyesha Kamala Harris akichuana vikali na Donald Trump, ambapo utafiti wa Reuters/Ipsos unamuonyesha akiongoza kwa asilimia 44 dhidi ya asilimia 43.
Utafiti mwingine unaonyesha Harris pamoja na mgombea mwenzake, Gavana wa Minnesota Tim Walz, katika kinyang'anyiro kikali kwenye majimbo muhimu ya ushindani kama Wisconsin, Pennsylvania, Georgia, Arizona, North Carolina, Michigan, na Nevada.