Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amemuagiza Mkurugenzi wa Idara ya Ufundi na Umeme (DTES), Mhandisi, Mwanahamisi Kitogo na Mtendaji Mkuu wa Vikosi vya Ujenzi, Mhandisi, Simeon Machibya kuhakikisha jengo la Wizara ya Ujenzi linakamilika kwa wakati na ubora uliokusudiwa.
Akizungumza jijini Dodoma leo Disemba 17, 2024 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo linalojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba, Waziri Ulega ameridhishwa na maendeleo yake ambalo hivi sasa limefika asilimia 80 na kumtaka Mkandarasi kuhakikisha jengo hilo linakuwa la mfano kwa ubora na mvuto.
Waziri Ulega amesisitiza umuhimu wa kutumia bidhaa za ujenzi zinazozalishwa hapa nchini pale inapowezakana ili kukuza viwanda na kuhamasisha biashara.
“Hakikisheni kwa zile bidhaa zenye ubora ambazo zinaweza kupatikana hapa nyumbani ni vizuri zinunuliwe hapa nyumbani, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa ya kuwaleta wawekezaji waje waanzishe viwanda mbalimbali za ujenzi, madawa hivyo soko la kwanza lazima iwe ni sisi wenyewe,” amesema Waziri Ulega.
Aidha, Ulega ametoa rai kwa Wizara kuwashirikisha wanafunzi kutoka vyuo vikuu na vyuo vya ufundi kupata mazingira ya kujifunza kwa vitendo ili kuwawezesha kupata uzoefu, weledi na kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika fani ya uhandisi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Vikosi vya Ujenzi, Mhandisi, Simeon Machibya amemhakikishia Waziri Ulega kutekeleza maagizo yake kwa kulijenga jengo katika viwango bora vinavyowezesha kukidhi mahitaji ya watu wote wakiwemo watu wenye mahitaji maalum.