Back to top

UMEME WA UHAKIKA NI AZMA YA SERIKALI KWA WANANCHI

03 February 2025
Share

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema ni azma ya Serikali kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika na unaotabirika kwa ajili ya shughuli za kijamii na  kimaendeleo. 

Mhe. Kapinga ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma  wakati akijibu swali la la Mbunge wa Lushoto Mhe. Shabani Shekilindi aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaondoa changamoto ya kukatika umeme katika Wilaya ya Lushoto kwa kuweka suluhisho la kudumu.

"Tutafuatilia kwa hii wiki moja kufahamu ni nini changamoto ya kukatika kwa umeme Wilaya ya Lushoto, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge iwapo kuna matengenezo tutahakikisha yanakamilika kwa haraka." Amesisitiza Mhe. Kapinga

Akijibu swali Mbunge wa Nkasi Kusini, Mhe. Vicent Mbogo aliyetaka kufahamu uwepo wa nishati ya umeme katika Kijiji cha Msamba-Masokolo, Lyapinda, Izinga na Lyele na katika Vitongoji vya Kisenga na Lupata, Mhe. Kapinga amesema Wilaya ya Nkasi ina jumla ya vijiji 90  ambapo vyote  vimepatiwa huduma ya umeme vikiwemo vijiji vya  Lyele na Lyapinda. 

Aidha, amesema Kitongoji cha Lupata kilichopo katika Kijiji cha Lyapinda kitapata umeme  kupitia mradi wa Vitongoji  15 vya Mbunge utakaotekelezwa na Mkandarasi aitwae M/s  STEG International Services Ltd ambaye ameshakamilisha  hatua za upimaji na usanifu. 

Ameongeza kuwa, uhakiki wa Kitongoji cha Kisenga umekamilika na Kitongoji hicho  kitapatiwa  umeme kupitia mradi wa vitongoji (HEP IIB).