Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kupokea tuzo ya “The Gates Goalkeepers Award” ikiwa ni kielelezo cha matokeo makubwa ambayo yamepatikana katika uongozi wake kufuatia ripoti ya utafiti wa demografia na afya ya mwaka 2022 inayoonesha kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi kwa kiwango cha asilimia 80 pamoja na Watoto wachanga.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo wakati akitoa taarifa ya upokeaji wa tuzo hiyo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zinazoandaliwa na taasisi ya The Gates Foundation, mbele ya waandishi wa habari katika ofisi za Wizara ya Afya, Jijini Dar es Salaam.
Waziri Mhagama amesema tukio hilo linafanyika nje ya Marekani katika nchi ya Tanzania kwa mara ya kwanza na Rais Samia ndiye kiongozi wa kwanza kupata tuzo hiyo kwa bara la Afrika jambo lililochagizwa na uongozi wake mahiri uliopelekea mafanikio makubwa nchini hususani katika sekta ya afya kwa kuitendea haki na kusababisha mataifa makubwa Duniani kutambua mchango wake.
Amesema kuwa mafanikio haya yametokana na mikakati mbalimbali iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa kufuatia utayari wa kisiasa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia kuweka mazingira wezeshi kisera pamoja na kuimarisha rufaa za akina mama na watoto.
“Pia Rais Samia ameweza kuongeza bajeti ya kuimarisha huduma ikiwemo upatikanaji wa madawa na vifaa tiba, kusogeza huduma za dharula za uzazi karibu na wananchi kwa kujenga zaidi ya vituo 530 vya upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni na kuendelea kuajiri watumishi wa afya hususani wanaotoa huduma za akina mama na Watoto,” amesema Waziri Mhagama
Waziri Mhagama ameishukuru Taasisi ya The Gates Foundation kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kupambana na vifo vitokanavyo na uzazi, Watoto wachanga na walio na umri chini ya miaka mitano (5), miradi ya Malaria, UKIMWI, chanjo, kifua kikuu na magonjwa yasiyopewa kipaumbele.
“Kwa namna ya kipekee, tunawashukuru kwa kutambua jitihada za kipekee za Amiri jeshi Mkuu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mapambano ya vifo vya kina mama vinavyotokana na uzazi, vifo vya Watoto wachanga na Watoto walio chini ya miaka mitano, hivyo wananchi wenzangu tunayo kila sababu ya kushukuru, kusheherekea na kutembea kifua mbele kwa jinsi Mheshimiwa Rais anavyotung’arisha nje ya mipaka ya nchi yetu,” amesema Waziri Mhagama