![](https://www.itv.co.tz/sites/default/files/styles/large/public/field/image/NDEJE_1.jpg?itok=7njjRDL2)
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi, amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Mandeleo ya Makazi, Mhanidisi Anthony Sanga, kuunda kamati mara moja kwa ajili ya kushughulikia mgogoro wa ardhi wa kiwanja namba 01, Kitalu R kilichopo barabara ya Nyerere Jijini Mwanza.
Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo baada ya kutembelea kiwanja hicho jijini Mwanza, alipofanya ziara mahususi kushuhudia na kusikiliza pande mbili za malalamiko baina ya mmiliki Z.E.K Ladhan Ltd na Halmashauri ya jiji la Mwanza.
Waziri Ndejembi ameagiza hadi kufikia Ijumaa Februari 14. 2025 kamati hiyo iwe tayari imepatikana, ikihusisha wajumbe kutoka Wizara Ardhi na Mkoa wa Mwanza.
Amesema kamati hiyo inapaswa kufanya kazi ya kupitia nyaraka kwa siku saba kuanzia Februari 17, 2025 na itoe mapendekezo ya nani mmiliki halali na nini kifanyike ili kumaliza mgogoro huo.
Aidha, Waziri Ndejembi ametoa wito kwa jamii kuendelea kufuata sheria wakati wanapotaka kumiliki ardhi ili kujiepusha na migogoro na kuwahimiza watumishi wa Sekta ya Ardhi kuendelea kufanya kazi kwa kufuata maadili ya utumishi umma kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayotolewa na Serikali.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema serikali ya mkoa anauongoza upo mstari wa mbele kuhakikisha migogoro ya ardhi mkoani humo namalizika ili wananchi waendelee kufanya shughuli za maendeleo.