
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete leo amezindua Bodi mpya ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na kuagiza Bodi hiyo kusimamia uwekezaji wa Mfuko wenye tija, kusimamia mipango ya Mfuko na kusimamia maadili.
Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi wa Bodi, Mhe. Waziri ameelekeza Bodi hiyo kusimamia Sera, Sheria, Kanuni, kuzingatia miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali pamoja na kusimamia misingi ya uwajibikaji, uadilifu, ubunifu na ushirikiano katika kazi.
"Misingi hii ni muhimu kwa sababu inahakikisha PSSSF inafanya kazi kwa ufanisi, usawa na haki, kuepuka rushwa kwa watumishi na viongozi katika kuhakikisha Mfuko unakua endelevu na kukuza uhimilivu wake," alisema Mhe. Kikwete.
Akitoa shukrani, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bi. Joyce Mapunjo alishukuru uteuzi wa wajumbe wa Bodi kwani umezingatia taaluma mbalimbali ambazo zitawezesha ustawi wa Mfuko pia aliipongeza utendaji kazi wa PSSSF.
"Wajumbe wa Bodi hii uteuzi wake umezingatia taaluma zote muhimu, kumekua na mchanganyiko mzuri tunaamini kazi itatendwa vizuri," alisema Bi. Joyce Mapunjo.
Alimhakikishia Mhe. Waziri kuwa Bodi mpya imepokea maelekezo yote aliyotoa na kuahidi kuwa wamejiwekea mikakati ya kutenda kazi kwa spidi ya kukimbia kuendelea pale ambapo Bodi iliyopita ilipoishia.
Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Abdul-Razaq Badru alisema Mfuko unaahidi kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na kuongeza kua Mfuko uko kwenye uelekeo mzuri, vitendea kazi na rasilimali watu ya kutosha.