Asilimia 90 ya madaraja yote ya reli ya Tanzania na Zambia, TAZARA, kwa upande wa Tanzania yamehujumiwa kwa kung'olewa vyuma na njia za waenda kwa miguu hali ambayo italigharimu taifa fedha nyingi kwa ajili ya kuyafanyia matengenezo ili yarejee katika hali yake ya kawaida.
Meneja wa usalama wa reli ya TAZARA kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam, Sadick Antony ameyasema hayo wakati wa zoezi la kutoa elimu kwa viongozi wa vitongoji, vijiji na kata zinazopitiwa na reli ya TAZARA ambalo limefanyika kwenye stesheni ya Malamba wilayani Mbarali ikiwa ni utekelezxaji wa agizo la naibu waziri wa uchukuzi na mawasiliano Mhe.Atashasta Nditiye alilolitoa hivi karibuni akiwa mkoani Mbeya.
Pamoja na uharibifu huo, mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa majini na nchi kavu, SUMATRA, umewahakikishia watanzania kuwa usafiri wa reli ya TAZARA bado ni salama ingawa hujuma hizo zikiendelea zitaliingizia taifa hasara kubwa.
Mwakilishi wa kamanda wa kikosi cha usalama wa reli ya TAZARA, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Jackson Mwakagonda ameagiza wananchi wote wanaomiliki vyuma vya reli ya TAZARA kuvirejesha mara moja kwenye stesheni za TAZARA zilizo karibu kabla jeshi la Polisi halijafanya operesheni kali ya kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria.