
Mahakama ya hakimu mkazi Mfawidhi mkoa wa Iringa imemkuta na kesi ya kujibu mwenyekiti wa mtandao wa wanafunzi nchini Abdul Nondo katika kesi inayomkabili.
Akisoma uamuzi mdogo wa mahakama hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo Mheshimiwa Liad Chamshama amesema kulingana na maelezo yaliyotolewa na Jamhuri pamoja na upande wa utetezi mahakama imemuona mshitakiwa Abdul Nondo anayo kesi ya kujibu katika maelezo yake aliyoyatoa kwa afisa wa polisi hivyo anatakiwa kuthibisha ukweli wa maelezo hayo.
Katika kesi ya jinai namba 13 ya mwaka 2018 Abdul Nondo anashitakiwa kwa makosa mawili ikiwemo kutoa taarifa ya uwongo kwa afisa wa polisi kituo cha polisi Mafinga akidai alitekwa na watu wasiojulikana na kumtelekeza katika kiwanda cha Pareto Mafinga maelezo ambayo Nondo anatakiwa kuyathibitisha mahakamani.