Back to top

Wananchi watahadharishwa na matumizi ya umeme nyakati za mvua.

13 May 2019
Share

Wakazi wa jiji la Dar es Salaam wametakiwa kuwa makini wanapotumia umeme kipindi hiki cha  mvua ili kuepuka athari zinazosababishwa na hitilafu na wakati mwingine kusababisha majanga ya moto.

Tahadhari hiyo imetolewa kwa nyakati tofauti kwa  ITV Online na Makamanda wa Mkoa wa jeshi la zimamoto na uokoaji wa Ilala Elisa Mugisha ,Kinondoni Juma Yange na Temeke Puyo Nzalamisi wakati wakitoa tathmini ya hali ilivyo na tahadhari ambazo wamezichukua mpaka sasa katika maeneo yao katika kipindi hiki cha mvua.

Wamesema mpaka sasa hawajapokea taarifa za madhara yoyote ila baadhi ya maeneo wamepata athari za mafuriko likiwemo eneo la Jangwani,mkwajuni  na vikosi kazi cha Jeshi hilo vipo maeneo hayo kwa usalama wa maisha ya watu.

Akizungumzia upande wa mkoa wa Ilala Kamanda Elisha Mugisha amesema wako jirani na wakazi wa eneo hilo hususani wakazi wa Jangwani ili kuzuia maafa kwakuwa ni moja ya maeneo yenye changamoto kubwa na kuwataka kuwa makini kwa maslai ya afya na maisha yao.