Watanzania wameungana na mataifa meengine duniani katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kutokomeza Homa ya Ini ambapo takwimu zinaonesha ugonjwa huo unaendelea kuongezeka nchini.
Kwa sasa kiwango cha Homa ya Ini kimefikia asilimia 4.5 na hakuna uelewa wakutosha miongoni mwa jamii.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa Jijini Dodoma katika Hospitali ya Benjamini Mkapa yame kwenda pamoja na zoezi la wananchi kujitokeza kupima na kupata chanjo ya Homa ya Ini.
Akizungumza katika zoezi hilo Kaimu Mkurugenzi wa Kinga, Wizara ya Afya Dkt.Janeth Mghamba amesema wizara imeweka mikakati ya kupunguza maambukizi mapya ya Homa ya Ini kwa asilimia 90 ifikapo 2030.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamini Mkapa, Dkt.Alphonce Chandika amesema hospitali hiyo imeshiriki katika maadhimisho hayo na tayari wananchi zaidi ya 400 na kati yao wagonjwa 13 wamegundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa wa Ini na kusema wamejipanga kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii pamoja na utoaji wa chanjo ya ugonjwa huo.