Back to top

Mwili wa kijana asiyefahamika wakutwa ukining'inia juu ya mti, Mbeya

09 May 2020
Share

Mwili wa kijana anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 23 na 25 umekutwa ukining'inia juu ya mti  katika mtaa wa RRM Isyesye, kata ya Isyesye jijini Mbeya akidaiwa kuwa amejinyonga kwa kutumia kamba na kusababisha taharuki kwa wananchi wanaishi kwenye eneo hilo.

Baadhi ya watu ambao wameshuhudia tukio hilo wamesema kuwa wameamka asubuhi ya leo na kushangaa kukuta mwili wa kijana huyo ambaye bado haujafahamika ukiwa unaning'inia juu ya mti na walipousogelea wakabaini kuwa mtu huyo ameshapoteza maisha ndipo wakaamua kutoa taarifa polisi huku wakiomba serikali kufanya uchunguzi ili kujua chanzo cha kifo hicho.

Kaimu mwenyekiti wa mtaa huo wa RRM Isyeye, Uswege Paulo Mwakalobo amesema hilo ni tukio la kwanza kutokea katika mtaa wake ambapo akawataka wananchi wanaofika kushuhudia tukio hilo wasisahahu kuchukua tahadhari ya maambukizi ya virusi vya Corona kwa kutosababisha msongamano.

Licha ya askari wa jeshi la polisi kufika katika eneo la tukio na kuuondoa mwili wa marehemu, lakini kamanda wa polisi mkoa wa mbeya, kamishna msaidizi mwandamizi wa jeshi la polisi Ulrich Matei  hakupatikana kuzungumzia tukio hilo.