Back to top

MASHAMBA YA TANZANIA PLANTATIONS LTD YAKABIDHIWA KWA SERIKALI

30 April 2022
Share

Serikali imekabidhiwa mashamba yaliyokuwa yakimilikiwa na Kampuni ya Tanzania Plantations Ltd yenye ukubwa wa ekari 6,176.5 katika Wilaya za Arusha na Arumeru mkoani Arusha na hivyo kumaliza mgogoro wa muda mrefu. 
 
Mgogoro kati ya Kampuni ya Tanzania Plantations Ltd na Serikali uliibuka mwaka 1999 baada ya kampuni hiyo kupinga ubatilisho wa mashamba yake uliofanywa na serikali kutokana na kampuni hiyo kushindwa kutimiza masharti ya umiliki jambo lililoifanya kufungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Arusha mwaka 2015.
 
Hata hivyo, katika kutafuta suluhu nje ya Mahakama Serikali kupitia Wakili Mkuu wa Serikali Mei 15, 2019 aliwasilisha ombi la kufanya majadiliano na mdai kwa lengo la kumaliza shauri nje ya mahakama ambapo Mahakama iliridhia pande mbili za shauri kumaliza suala hilo nje ya mahakama.

Makabidhiano ya mashamba hayo yaliyokuwa yakijulikana kama Karangai na Lucy Estate yanahitimisha mgogoro kati ya serikali na Kampuni ya Tanzania Plantations Ltd sambamba na ule wa wananchi uliotokana na wananchi kuuziwa baadhi ya maeneo kwenye mashamba yaliyobatilishwa.
 
Katika makubaliano ya kutafuta suluhu nje ya mahakama, Serikali ilikubali kulipa shilingi bilioni 5.7 kwa ajili ya fidia ya mashamba Na 304 na 305  Nduruma yenye ukubwa wa ekari 6,133 na shamba la ekari 43.5 ambalo halikubatilishwa lakini ilionekana ni busara likachukuliwa na serikali. Pia serikali ililipa fidia ya mkonge na mtambo wa kuchakata mkonge uliokuwa ukifanya kazi.
 
Makabidhiano ya mashamba hayo yamefanyika katika kata ya Bwawani wilayani Arumeru mkoani Arusha baina ya Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi na Mkurugenzi wa Tanzania Plantation Ltd Bw. Ladhia Prabhudas Pradip.