Asilimia 34 ya watoto nchini wenye umri chini ya miaka mitano wanakabiliwa na tatizo la lishe duni hali inayosababisha udumavu wa akili kwa kiwango kikubwa ambapo wanakuwa na uwezo mdogo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotakiwa kutumia akili.
Katibu mkuu wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia,wazee na watoto Dkt.Mpoki Ulisubisya ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizindua vitini vilivyoandaliwa na taasisi inayojishughulisha na masuala ya afya katika nchi zilizopo Mashariki,kati na kusini mwa Afrika vyenye lengo la kuboresha utoaji huduma za lishe katika ngazi ya vituo vya afya na kwenye jamii ambapo amesema hayo yamebainika baada ya tafiti mbalimbali zilizofanywa.
Mtaalamu wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza,lishe na usalama wa chakula wa taasisi hiyo Bi. Rosemary Mwaisaka amesema katika utafiti uliofanyika katika nchi tatu za Afrika Mashariki imebainika kuwa watu wengi hawaelewi umuhimu wa suala la lishe wakiwemo watendaji na watoa huduma katika jamii.
Kitabu hicho cha kusaidia muongozo wa lishe kinatarajiwa kutumika na watenda kazi walio mstari wa mbele katika maeneo mbalimbali yakiwemo wizara ya afya,kilimo, elimu na maendeleo ya jamii.