Asilimia kubwa ya magari hasa yanayobeba mizigo yamebainika kubadilishwa mifumo yake na kufungwa vifaa bandia na yanafanyakazi nje ya mifumo yake ya kawaida jambo linalochangia yashidwe kumudu changamoto za barabarani hasa kwenye maeneo ya miinuko na miteremko mikali.
Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Arusha Bw Ramadhani Nga'anzi baada ya kuongoza oparesheni ya ukaguzi wa magari ya abiria na mizigo zoezi ambalo limebainisha mapungufu mbalimbali yanayoonekana kwa macho na yanayoweza kurekebishwa katika taratibu za kawaida na yanayohitaji utaalam kulingana na aina magari yanayotumika.
Kufuatia hali hiyo Kamanda Ramadhani Ng'anzi amesema kuna haja ya wadau wengine wakiwemo wataaam waliobobea kwenye mifumo ya vyombo vya moto kufuatilia kwa undani utengenezaji wa vyombo hivyo kwani yapo mapungufu mengi yaliyijificha kama hatua ya kuunga mkono jitihada zinazoendelea za kukabiliana na ongezeko la ajali.
Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani mkoa wa Arusha Bw Joseph Bukombe amewaomba wamiliki wa magari kubadilisha mtazamo wa kutumia gharama kubwa kupamba magari yao kwa rangi nzuri za kuvutia badala yake waelekeze nguvu kutengeneza na kuimarisha mifumo ya ndani suala ambalo lina tija kwao wenyewe na abiria kwa ujumla.