Back to top

Bilioni 2 zatengwa kwa wananchi watakaovamiwa na wanyama pori.

27 April 2021
Share

Serikali imesema imetenga shilingi bilioni mbili katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kifuta jasho kwa wananchi wote watakaovamiwa na wanyama pori.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Mary Masanja amesema hayo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Namtumbo Mhe.Vita Kawawa aliyetaka kujua mikakati ya serikali katika kufidia wananchi wanaoshambuliwa na wanyama pori ikiwemo Tembo.

Mhe.Masanja amesema serikali itatoa fidia kwa wananchi wote watakaovamiwa na wanyama kulingana na uharibifu utakaojitokeza.

Wakati huo huo, serikali imesema itaendelea kuboresha na kukarabati wa miundombinu ikiwemo barabara, madaraja na mifereji ya mvua jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri Ofisi  ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mita (TAMISEMI) Mhe.David Silinde amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe.Felister Njau aliyetaka kujua mkakati wa serikali katika kusaidia wananchi wa Mbweni, Tegeta na Ununio  ambao mara nyingi wamekuwa wakikubwa na mafuriko hasa nyakati za mvua.

Mhe.Silinde amesema pamoja na mikakati hiyo ya serikali wanatambua changamoto ya mafuriko katika maeneo mbalimbali nchini na kuwa maeneo yote korofi yatafikiwa na serikali.