Back to top

BITEKO AZINDUA KITUO CHA KUPOZA UMEME GGM.

13 August 2024
Share

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amezindua kituo cha kupokea na kupoza umeme katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), chenye uwezo wa Megawati 34 ambacho sasa kinawezesha GGML, kuanza kutumia umeme wa gridi kwa matumizi yake badala ya mafuta na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji.

Baada ya kuzindua kituo hicho wilayani Geita mkoani Geita, Dkt.Biteko amesema ujenzi wa kituo hicho, ni alama halisi ya umoja na ushirikiano uliopo kati ya Serikali na Sekta Binafsi, kwani mradi huo umehusisha ujenzi wa laini ya umeme ya Kv 33, ambayo imejengwa na TANESCO kwa gharama ya shilingi bilioni 8.04 huku GGML ikijenga kituo cha kupoza umeme kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 24.

Amesema GGM ilikuwa inatumia shilingi bilioni 130 kwa mwezi kama gharama za uendeshaji na kwenye umeme wa mafuta ilikuwa inatumia shilingi bilioni 13.4 kila mwezi na kuathiri mapato yake kwa Serikali.


Vilevile, ameipongeza GGM kwa kuzipa kipaumbele kampuni za kizawa katika kutoa huduma kwenye mgodi huo na kusisitiza kuwa huo ndio msimamo wa Serikali ya Tanzania wa kuhakikisha kampuni za ndani zinapewa kipaumbele kwenye miradi mbalimbali.

Dkt.Biteko amewaagiza Watendaji wa Wizara ya Nishati, TANESCO na Taasisi nyingine za Serikali, kujali sekta binafsi kutokana na manufaa yake ikiwemo kuwa walipakodi wakubwa na kuongeza ajira nchini.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio, amesema hali ya umeme nchini kwa ujumla ni nzuri huku uzalishaji ukikidhi mahitaji na ziada kidogo.

Kuhusu usambazaji umeme mkoani Geita amesema kuwa Mkoa una Vijiji 486 na kati ya hivyo vijiji 483 vina umeme sawa na asilimia 99.38.

Ameongeza kuwa, kazi ya kupeleka umeme katika vitongoji mkoani Geita, inaendelea ambapo kati ya vitongoji 2,197, vitongoji takriban 1000  tayari vina umeme.