Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amesema Serikali inatarajia kujenga chumba maalum cha kuhifadhi baridi katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Songwe kwa ajili ya kuhifadhia maparachichi pamoja na mazao mengine kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.
Kauli hiyo ya Waziri Mkuu Majaliwa ameutoa baada ya kutembelea shamba la mkulima wa Parachichi Bwana Steven Mlimbira katika kijiji cha Maheve wilayani Njombe.
Ameziagiza Halmashauri zote za mkoa wa Njombe zinazolima zao la parachichi zianzishe vitalu vya kuotesha miche katika eneo la kuanzia ekari tatu na kuigawa bure kwa wakulima lengo likiwa ni kuhamasisha wananchi wengi kulima zao hilo na kuongeza uzalishaji.
Ameeleza kuwa zao la parachichi ni miongoni mwa mazao yenye faida kubwa na linazalishwa kwa gharama nafuu, hivyo amewahimiza wananchi kote nchini kulima zao hilo kwa ajili ya kujipatia fedha zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi.
Kadhalika amesema zao la parachichi limechangia katika kutatua tatizo la ajira nchini ambapo watu wengi wameweza kujiajiri na kuajiriwa, hivyo ametoa wito kwa Watanzania kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata zao hilo kwa kuwa linafaida kubwa.