#HABARI: Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, amedhamiria kuboresha miundombinu ya ufugaji ili wafugaji wafuge kisasa wakiwa katika maeneo yao rasmi na kuondokana na ufugaji wa kuhamahama.
Dkt.Kijaji amesema kufuatia mpango huo Wizara ya Mifugo na Uvuvi inadhamiria bajeti zake za fedha za kila mwaka zitoe vipaumbele kwenye malisho ya mifugo na maji ili kuwaondolea adha wafugaji kutotembea muda mrefu kufuata mahitaji hayo muhimu kwa ajili ya mifugo yao.
Mhe. Dkt. Kijaji amebainisha wakati wa kikao chake na baadhi ya wafugaji katika Wilaya ya Mvomero, Mkoani Morogoro ambapo amesema katika kuhakikisha hilo ni lazima wakuu wa mikoa wahamasishe mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Ameeleza kuwa katika Mwaka wa Fedha 2025/26 serikali itakuja na mpango kwa ajili ya kuchimba visima na mabwawa ili kuwahudumia wafugaji na mifugo yao kote nchini.
Ameongeza kuwa vituo atamizi na mbegu bora za mifugo ndiyo chachu kwa Tanzania kuwa na nafasi kubwa ya kuuza mazao ya mifugo nje ya nchi na kuondokana na vikwazo vya kimataifa ambavyo imekuwa ikikabiliana navyo juu ya ubora wa mazao hayo yanapotakiwa katika nchi hizo.
Baadhi ya wafugaji waliohudhuria kikao hicho wamempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan namna Serikali ya Awamu ya Sita inavyoleta matokeo chanya kwa wafugaji kwa kuwahimiza kufuga kisasa na kuwasogezea huduma mbalimbali karibu na maeneo hayo.