Back to top

HUDUMA ZA KISHERIA KUMPA AHUENI MWANANCHI

05 September 2024
Share

Wizara ya Katiba na Sheria imeanzisha Kituo cha Huduma Kwa Mteja, kwa ajili ya Huduma za kisheria baada ya kubaini kuwa malalamiko mengi ya wananchi yamekuwa yakiwasilishwa wizarani kwa njia ya Barua au kufika moja kwa moja kwenye Ofisi za Wizara kwa kutumia gharama kubwa.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi ameeleza hayo Jijini Dodoma na kubainisha kuwa kituo hicho kitawezesha kupokea Taarifa na malalamiko yanayohusu tuhuma za rushwa, ukiukwaji wa haki unaofanywa na Taasisi ama mtu mmoja mmoja, na maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusiana na huduma zinazotolewa na Wizara ya Katiba na Sheria, pamoja na Taasisi zote zilizo katika mnyororo wa haki.

Waziri Kabudi amesema uwepo wa Kampeni ya msaada wa Kisheria ya Mama Samia, ambayo inaendeshwa na Wizara katika maeneo mbalimbali nchini, imeleta hamasa kubwa ya wananchi kuwasilisha malalamiko na hoja mbalimbali za kisheria ambazo zinahitaji ufumbuzi wa haraka.

Hadi kufikia 31, Agosti 2024 jumla ya malalamiko 499 yamesajiliwa, kati ya hayo 410 sawa na asilimia 82 yamefanyiwa kazi Kwa ukamilifu na 89 ambayo ni asilimia 18 yako katika hatua mbalimbali za kutafutiwa ufumbuzi.