Back to top

MOROGORO, NJOMBE NA RUVUMA KUUNGANISHWA KWA KIWANGO CHA LAMI

05 August 2024
Share

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwa Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara zinazounganisha Mkoa wa Morogoro na Mikoa ya Njombe na Ruvuma kwa kiwango cha lami.

Dkt. Samia ameeleza hayo wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa upanuzi wa kiwanda cha kuzalisha sukari cha Kilombero, Mkoani Morogoro.

“Mikoa ya Morogoro, Njombe na Ruvuma ni maeneo ambayo yanatoa chakula kingi sana na ni lazima tuhakikishe miundombinu inakuwa bora ili tuweze kutoa chakula kiende kwenye Soko, kwahiyo ni ahadi yetu na kama mnavyojua tukiahidi tunatenda”, amesema Dkt. Samia.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa ameeleza kuwa ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara (km 66.9) kwa kiwango cha lami na Daraja la Ruaha Mkuu (m 133) umegharimu kiasi cha shilingi Bilioni 157.15.

Bashungwa ameongeza kuwa ukamilikaji wa barabara ya Kidatu – Ifakara (km 66.9) na Daraja la Ruaha Mkuu unaenda kuleta mageuzi ya kiuchumi kwa Mkoa wa Morogoro na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na Mikoa ya Kati kwa kuwa barabara hii inaunganisha Mkoa wa Morogoro na Mikoa ya Njombe, Ruvuma na Lindi kupitia Wilaya ya Kilosa, Kilombero, Ulanga na Malinyi zenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula.

Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, ameeleza kuwa barabara ya Kidatu - Ifakara (km 66.9) na Daraja la Ruaha Mkuu imejengwa kwa kuzingatia viwango vya usanifu kwa mujibu wa mkataba ambapo ujenzi ulianza tarehe 02 Oktoba 2017 na kukamilika 30 Juni, 2024 kwa gharama ya Shilingi Billioni 157.15 ikijumuisha ujenzi, usimamizi na fidia ya mali zilizoathiriwa na mradi.