![](https://www.itv.co.tz/sites/default/files/styles/large/public/field/image/kukuuu.jpg?itok=uMfG7rFI)
Mwanafunzi wa shule ya Msingi Kwamngumi wilayani Handeni amefariki kutokana na majeraha aliyoyapata kichwani baada ya kupigwa akituhumiwa kuiba kuku.
Akielezea tukio hilo ambalo limetokea mtaa wa Magari mabovu babu wa marehemu amedai kuwa ilikua majira ya saa mbili usiku wakati mjukuu wake akiwa katika matembezi ya kawaida ndipo akakutana na mkasa huo.
Kamera ya ITV ilifika Hospitali ya wilaya ya Handeni ambako mwili wa marehemu umehifadhiwa huku Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo Dkt. Hudi Shedadi akikiri kumpokea kijana huyo na kudai kuwa amefariki kutokana na majeraha ya kichwani.
ITV iliweza kuongea na kamanda wa polisi mkoa wa tanga na amesema kuwa tayari Jeshi la Polisi limeanza kuchukua hatua kwa waliofanya kitendo hicho huku Mkuu wa wilaya ya Handeni Godwin Gondwe akiwataka wananchi kuacha kuchukua sheria mkononi.