Back to top

NDEJEMBI AAGIZA SHUGHULI ZA UJENZI ZISITISHWE NDACHI

05 September 2024
Share

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi, ameagiza kusitishwa kwa shughuli za ujenzi katika eneo la Ndachi Jijini Dodoma,  ambalo limekua likikabiliwa na mgogoro wa muda mrefu.

Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo wakati wa kikao chake cha pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe Rosemary Senyamule, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabir Shekimweri, Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dodoma, Wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi pamoja na wale wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kilichokua na lengo la kujadili ufumbuzi wa mgogoro huo.

Mhe. Ndejembi ameelekeza kuwa, ujenzi wowote katika eneo hilo, usimame kwa sababu kadri unavyozidi kufanyika bila kibali cha ujenzi ndivyo mgogoro unavyozidi kukua.

Aidha, Mhe. Ndejembi amemuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga, kuunda timu ya wataalam kutoka wizarani watakaoshirikiana na watalaamu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya pamoja na Halmashauri ili kufanyia tathmini mgogoro huo na kuupatia ufumbuzi na ndani ya siku saba timu hiyo iwe imeanza kazi hiyo.