Kuelekea siku ya wanawake duniani, ambayo kilele chake ni Machi 8, 2024, Jeshi la Polisi mkoani Morogoro limepanda miti 500 katika Kambi za Polisi pamoja na makazi jirani,zoezi litakalodumu wiki nzima katika maeneo mbalimbali nchini.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro ACP Alex Mkama amesema ameongoza zoezi la upandaji miti kwa Maofisa wakaguzi na Askari katika kambi za Polisi na maeneo jirani ili kuleta mandhari nzuri, kivuli na kulinda ardhi dhidi ya mmomonyoko.
ACP Mkama amesema, zoezi la upandaji miti linafanyika Tanzania nzima kufuatia maelekezo ya Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Camilius Wambura pamoja na Serikali hivyo hawanabudi kuyatekeleza kwa ukubwa wake.
Zoezi hili pia limeshirikisha Wachezaji wa mpira wa miguu ya Mbeya city inayoshiriki ligi ya Championship ambao wanaofanya mazoezi kwenye uwanja wa Polisi uliopo kwenye kambi za Polisi Morogoro.
Pius Joseph, Mchezaji wa Mbeya city amesema ni mara ya kwanza wanaalikwa na Jeshi la Polisi kushiriki zoezi la kijamii kwao imekuwa faraja na imewapa nguvu ya kwenda kupambana na kupata ushindi kwenye mchezo wao unaofuatia.