Back to top

SERIKALI HAITAPUUZA MCHANGO WA ASASI ZA KIRAIA: DKT BITEKO

06 September 2024
Share

 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amesema kuwa Serikali haitapuuza mchango wa asasi za kiraia, kwa kuwa wao ni wadau muhimu na wamekuwa wakishirikiana na Serikali katika kuwaletea Watanzania maendeleo.

Dkt.Biteko amesema hayo Jijini Dodoma, wakati akihutubia Mkutano wa Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.

"Serikali haitapuuza hata kidogo mchango wenu asasi za kiraia wala kuudogosha kwenye maendeleo ya nchi yetu kwenye nyanja zote ikiwemo za kiuchumi, utawala bora na kijamii kwa sababu ni wadau muhimu, mashirika yote yaliyopo nchini 9,777 yanalenga kuwahudumia Watanzania" Amesema Dkt. Biteko.

Ameendelea kwa kusema kuwa kazi ya Serikali ni kuhudumia Watanzania, ambapo pia kazi ya mashiriki hayo ni kuisaidia Serikali kuweza kutekeleza majukumu yake kwa urahisi na kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi  na kuwa hayapaswi kuwa adui wa Serikali bali mshirika na  mdau muhimu wa maendeleo.

Ametaja faida zingine za mashirika hayo kuwa ni fedha zilizopatikana ambazo ni shilingi trilioni 2.6 zimezunguka nchi nzima na zaidi ya watu 21,000 wameajiriwa katika sekta hiyo na kuwa yamekuwa yakichagiza jitihada za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi na afua mbalimbali hususan katika nyanja za afya, kilimo, elimu, maji na sekta nyingine mtambuka pamoja na kuchangia  kuboresha utoaji wa huduma za kijamii, kuongeza fursa za ajira hasa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu  na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

"Serikali inategemea kuwahudumia Watanzania katika kila afua mfano afya na hivyo wahudumieni kwa upendo nao watawafurahia na kushirikiana nanyi mahali mlipo"Amesisitiza Dkt. Biteko.

Ametaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuboresha mazingira ya utendaji kazi na kuongeza utambuzi wa mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuwa ni pamoja na kuandaliwa kwa Mwongozo wa Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania Bara (2020) ambao upo kwenye mapitio, Mfumo wa Kielektroniki wa Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (2020).