Ili kuondokana na changamoto za upangaji vijijini, Serikali kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeandaa wa mwongozo wa upangaji makazi na ujenzi wa nyumba Vijijini.
Ingawa upangaji wa vijiji na ujenzi wa nyumba bora vijijni unapaswa kuhusisha watu wote, serikali imeona ni vyema kutoa muongozo kwa kutumia lugha rahisi inayoeleweka kuelezea kanuni muhimu za kuzingatiwa na mamlaka na wana kijiji katika kupanga makazi ya vijiji bila kutegemea kutoka kwa wataalamu.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula, katika kikao kazi cha kujadili na kuweka mikakati wa kukwamua zoezi la urasimishaji makazi kilichofanyika mkoani Mbeya.
Kwa mujibu wa Dkt.Mabula, miongozo iliyozingatiwa katika uandaaji mwongozo huo ni pamoja na uandaaji wa mipangokina ya makazi vijijini pamoja na mwongozo wa utoaji vibali vya ujenzi na usimamizi wa ujenzi wa majengo kwenye mamlaka za serikali za mitaa wa mwaka 2018.
Amesema, eneo la Makazi la Kijiji ni sehemu ya mpango wa jumla wa Matumizi ya Ardhi ya kijiji unaoainisha maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali kama vile makazi, biashara, taasisi, kilimo , misitu , malisho ya mifugo na huduma za jamii na miundombinu.