Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Mashimba Ndaki, amewaagiza viongozi na watendaji wote mkoani Morogoro, kutowazuia wafugaji wanaohama kutoka bonde la Mto Kilombero ambapo amesema kuwa kufanya hivyo ni kukwamisha, utekelezaji wa agizo la Serikali linalowataka wafugaji na wakulima kuondoka kwenye bonde hilo.
Katika kutekeleza agizo hilo, Mhe.Ndaki amewasisitiza viongozi wa maeneo yenye wafugaji wanaopaswa kuhama, kuhakikisha wanawatafutia wafugaji hao maeneo ya kuhamia ili zoezi hilo la kuwahamisha lisiathiri shughuli zao za ufugaji.
Mhe.Ndaki ameeleza hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya sekondari Nakaguru, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba mkoani Morogoro ambao ulijumuisha wafugaji na wakulima wanaozungukwa na bonde la Mto Kilombero.
Akielezea namna watakavyotekeleza maagizo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe.Danstan Kyoba, ameahidi kukutana na viongozi na watendaji mbalimbali wa Wilaya hiyo kwa ajili ya kuanza kutenga maeneo, ambayo watahamia wafugaji na wakulima wanaoondoka kwenye bonde la mto Kilombero.
Bonde la Mto Kilombero linazungukwa na vijiji 23 vilivyopo Wilayani Kilombero, ambavyo ni Luwembo, Maulanga, Miwangani, Namwawala, Idandu, Kalenga, Kikwambi, Mofu, Miyomboni, Nakagulu, Ijia, Isago, Luvilikila, Mkangawalo, Chita, Melela, Chisano, Karangekelo, Msolwa, Miembeni, Kibugasa na Ngalimila.