Wananchi waliokuwa wamekumbwa na janga la mafuriko katika wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro wanalazimika kulala chini ya miti na watoto wao baada ya makazi yao ya muda waliyojenga kuharibiwa na upepo na wameiomba serikali na wadau wengine kuwasaidia.
Wakizungumza wakati wanapokea misaada vikiwemo vyakula magunia 300 ya Mahindi na Maharagwe iliyotolewa na kanisa katoliki jimbo la Same wananchi hao pamoja na kuwashukuru wamesema kukosekana kwa makazi kunabasababisha vitu wanavyopewa kuharibika.
Wamesema pamoja na kulalamikia makazi pia watoto wao wanaathirika kielimu baada ya shule iliyokuwa imekumbwa na mafuriko kufungwa na wanafunzi kuhamishiwa kwenye shule nyingine ambapo wanalazimika kusoma nusu siku tofauti na ilivyokuwa awali.
Askofu wa kanisa katoliki jimbo la Same Bw. Rogati Kimario amewaomba watanzania wenye mapenzi mema kujitolea kuwasaidia wananchi hao hasa suala la makazi na kuhusu changamoto ya elimu mkuu wa wilaya hiyo Bi.Rosemary Senyamule amesema utatuzi wake umeshaanza.
Wananchi hao zaidi wanaotoka kwenye zaidi ya kaya 800 walihamishiwa katika eneo hilo baada ya makazi yao kuzingirwa na maji ya mafuriko yaliyosababishwa na kujaa kwa bwawa laNnyumba ya Mungu mwezi mei mwaka huu 2018