Back to top

Wakazi wa Kasamwa mkoani Geita wajenga Chumba cha upasuaji.

03 April 2018
Share

Zaidi ya watu laki moja na elfu hamsini wa tarafa ya Kasamwa  waliokuwa wanalazimika kutembea zaidi ya kilometa ishirini na tano kufuata huduma ya upasuaji kwenye hospitali ya mkoa wa Geita wameondokana na adha hiyo baada ya kukamilika kwa ujenzi wa chumba cha upasuaji kwenye kituo cha afya Kasama kilichojengwa kwa nguvu za wananchi na fedha za mapato ya ndani za halmashauri ya mji wa Geita ujenzi unaoenda pamoja na ujenzi wa kisima kirefu cha maji katika eneo hilo.

Wakizungumza katika tukio la uzinduzi wa chumba hicho cha upasuaji katika kituo cha afya Kasamwa wakazi wa eneo ilo wanasema wameteseka kwa muda mrefu kutokana na kukosekana kwa huduma hiyo hasa kwa wanawake wajawazito wanaoshindwa kujifungua kwa njia ya kawaida.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya mji wa Geita Apolinary Modest anasema huduma hiyo itasaidia wakazi kutoka zaidi ya vijiji ishirini na tatu kutoka kata tano ambao kwa muda mrefu wameikosa huduma hiyo muhimu kwa binadamu.

Akizindua mradi huo pamoja na miradi ya maji, jengo la utawala la halmashari ya mji wa Geita na kugawa vyandarua kwa zaidi ya wanawake miamoja wajawazito na wenye watoto  wachanga kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa 2018  Charles Kabeho anasema haya ni matunda ya utendaji wa serikali ya awamu tano.