Back to top

WALIOATHIRIWA NA WANYAMA WAKALI KUFUTWA MACHOZI

04 November 2022
Share

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Mary Masanja, amesema Wizara hiyo imeanza kufanya tathimini, ili iweze kutoa kifuta machozi kwa wananchi walioathiriwa na uvamizi wa wanyama wakali, na waharibifu kwenye maeneo yao na kwamba utekelezaji wake unatarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Mhe.Mary Masanja ametoa kauli hiyo Bungeni Dodoma, wakati akijibu maswali ya wabunge juu ya hatua zinazochukuliwa na serikali kuhusu wananchi wanaokabiliana na uvamizi wa wanyama wakali.

Mhe.Masanja, amesema katika kudhibiti hali hiyo, ujenzi wa vituo vya askari karibu na maeneo ya wananchi umeanza, ili wananchi waweze kutoa changamoto zao na kupatiwa huduma kwa urahisi na haraka zaidi inapohitajika.

Aidha ameongeza kuwa serikali imeanza kutoa mafunzo kwa vijana kwenye maeneo husika, hususani Vijijini watakaoshirikiana na askari kudhibiti wanyama wakali, wanaposogea katika makazi na maeneo yenye shughuli za kibinadamu, ili iwe rahisi kuwaondoa.