Back to top

WANANCHI TUMIENI TAASISI RASMI ZA FEDHA

21 August 2024
Share

Ili kupunguza migogoro kati ya wananchi na watoa huduma ndogo za fedha, wananchi wa Halmashauri ya Mlimba, Wilayani Kilombero, Mkoani Morogoro, wameshauriwa kujielekeza kupata huduma hizo katika Taasisi za fedha ambazo ni rasmi na zilizosajiliwa na kupewa leseni ya kuendesha shughuli hizo.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlimba Neuster Ngelela, wakati akizungumza katika program ya elimu ya fedha inayoendeshwa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya Fedha nchini. 
 


Bi. Ngelela amesema kuwa kutokana na kasi ya maendeleo nchini, kila mtu amekuwa na uhitaji mkubwa wa pesa, hivyo kuwasihi wananchi wa Halmashauri ya Mlimba na Tanzania kwa ujumla kuhakikisha pesa wanazozipata wanazitunza kwa ajili ya maisha ya baadae, na hata wakiamua kukopa basi wakope kwa ajili ya kujiletea maendeleo.
 
Akiongea katika program hiyo, Diwani wa Viti Maalum wa Halmashauri ya Mlimba, Mhe. Reniter Limba aliwashukuru waratibu wa program kwa elimu waliyoitoa kwa wananchi wa Halmashauri hiyo ambayo kwa namna moja au nyingine itasaidia kupunguza wimbi la utapeli lililokuwa linafanywa na watoa huduma za fedha ambao si waaminifu kwa kutoa mikopo yenye riba kubwa na kusababisha wananchi washindwe  kurejesha na kuleta taharuki katika familia.
 
Programu ya kutoa elimu ya Fedha kwa Umma imeandaliwa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya Fedha nchini, ikiwa ni moja ya maeneo ya kipaumbele katika utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Mwaka 2020/21-2029/30.