Back to top

Wananchi wataka serikali iunge mkono ujenzi wa madarasa Uvinza

24 December 2018
Share

Wananchi wa wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma wameanza jitihada za kuwanusuru zaidi ya watoto elfu tatu na mia mbili ambao wamefaulu lakini hawataweza kuanza kidato cha kwanza kwa sababu shule 12 za sekondari hazina vyumba 84 vya madarasa.
 

Wamesema katika baadhi ya kata tayari wananchi wameanza kujitolea kujenga vyumba vya madarsa ambayo yamefikia katika hatua tofauti na kinachotakiwa sasa ni halmashauri na serikali kuwasaidia ili kukamilisha na hivyo kuwawezesha watoto kuendelea na elimu ya sekondari badala ya kukaa nyumbani.
 
Mkurugezi wa halmashauri ya Uvinza Weja Ng'olo amesema tatizo hilo ni kubwa na kwamba shule 12 hazijapangiwa kupokea watoto wa kidato cha kwanza mwakani kutokana na ukosefu wa vyumba vya madarasa na madawati ambapo amesema jitihada zinatakiwa kufanywa na madiwani ,wananchi na serikali katika kila kata ili kumaliza tatizo hilo.

Kati ya wanafunzi 4,057 waliofaulu katika wilaya ya Uvinza ni watoto 789 tu sawa na asilimia ishirini ndio wamepata nafasi ya kuchaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari huku zaidi ya elfu tatu wakikwama kwa sababu ya vyumba vya madarsa na madawati.