Back to top

Watalii kutoka mataifa mbalimbali waanza kutua Tanzania.

23 May 2020
Share

Ndege kutoka mataifa mbalimbali zimeanza kuwasili nchini zikiwemo za watalii ikiwa ni siku sita baada ya serikali kutangaza rasmi  kuondoa zuio la ndege kutua nchini lililokuwa limewekwa kutokana na tatizo la virisi vya Corona.
  
Ndege zilizoanza kuwasili zikiwa na watalii ni pamoja na zinazotoka Marekani na Afrika Kusini ambazo zimeanza kuingia nchini kupitia  uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro.
 
ITV imeshuhudia moja ya ndege kutoka Marekani ikitua katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro ikiwa na watalii ambao baada  ya kukamilisha taratibu za kiafya wameanza safari ya kwenda kuangalia vivutio katika maeneo mbalimbali. 
 
Wakizungumzia hatua hiyo mmoja wa watalii kutoka Afrika Kusini Tracu Stanley na rubani wa ndege ya watalii amesema amefurahi kupata fursa ya kuja nchini kujionea vivutio na pia ameridhishwa na tahadhari za kiafya zinazochukuliwa.

Kuanza kuwasili kwa watalii hao ni matokeo ya hatua ya serikali ya kufungua anga lake lililokuwa limefungwa kwa sababu ya tahadhari  za kuenea kwa virusi vya Corona ambapo Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Issack Kamwelwe amesema ndege zote za kibiashara, misaada, Kidiplomasia, dharura na ndege maalumu zinaruhusiwa kuruka, kutua na kupita kwenye anga ya Tanzania.