Back to top

WAZIRI BASHUNGWA:MPASUKO BARABARA YA BUSUNZU, SIO UPIGAJI.

10 July 2024
Share

Waziri wa Ujenzi Mh. Innocent Bashungwa, amesema kuwa uchunguzi umebaini mpasuko wa ardhi na kuporomoka kwa tuta la barabara, uliojitokeza katika eneo la Busunzu lenye urefu wa mita 200 haijatokana na makosa ya Mkandarasi kwenye ujenzi, bali umesababishwa na sababu za kijiolojia.

Bashungwa ametoa taarifa hiyo mkoani Kigoma, mara baada ya kukagua eneo hilo na kupokea taarifa ya uchunguzi iliyofanywa na Wataalamu wa miamba, kutoka Taasisi ya Geolojia na utafiti wa madini Tanzania (GST), Kitengo maalum cha Utafiti cha TANROADS, na School of Mines and Geosciences (SoMG) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Nimepokea taarifa za kitaalamu na nimejionea zaidi ya mita 200 namna ambavyo majanga ya asili yaliyoathirika eneo hili, Serikali iliunda jopo la kufanya utafiti wa kina kuanzia mwezi Februari na tulichokigundua hapa sio makosa ya Mhandisi, sio upigaji kama watu wengine walivyodhani”, amesema Bashungwa.

Bashungwa ameitaka TANROADS kuendelea kutekeleza Ushauri uliotolewa na Wataalamu hao waliofanya uchunguzi huku akielekeza TANROADS kuhakikikisha wanafanya usanifu wa barabara kwenye maeneo korofi wakati wa mvua kwa kushirikiana na Wataalamu wa Miamba ili kubaini tabia za maeneo hayo na kuepuka changamoto zinazojitokeza.


Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta amemueleza Waziri Bashungwa kuwa baada ya utafiti huo kufanyika hivi sasa Mhandisi Mshauri anaandaa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina utakaotoa michoro na gharama za matengenezo.

Mhandisi Besta ameeleza kuwa baada ya taarifa za Wataalamu wa miamba wameshauri kurudisha barabara sehemu ile ile iliyokuwa imejengwa awali ikiwa ni pamoja kujenga upya tuta la barabara la mita 270 pamoja na kujenga surface na subsurface drainage ili kuruhusu maji yapite bila kuathiri tuta la barabara.


Itakumbukwa mnamo mwezi Februari, 2024 Mkoani Kigoma katika mradi wa barabara ya Mvugwe - Makutano ya Nduta palijitokeza nyufa ndogondogo na baadae kipande cha barabara hiyo kuongezeka kutoka mita 50 hadi kufikia mita 200 na kuporomoka chini kına cha mita 15 kutoka usawa ilipojengwa awali.