Back to top

Zanzibar kuendeleza uhusiano na Oman.

09 March 2022
Share

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano kati yake na Oman na kuishauri nchi hiyo kuunga mkono Sera ya Uchumi wa Buluu ambayo ndio Dira ya uchumi wa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Sayyid Badr bin Hamad bin Hamood Al Busaid.

Dk. Mwinyi alimueleza Waziri Al Busaid kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini uhusiano na ushirikiano wa kihistoria kati yake na Oman hivyo, inawakaribisha wafanyabiashara, wawekezaji na wenye viwanda wa nchi hiyo kuja kuekeza Zanzibar hasa katika sekta za uchumi wa Buluu.

Rais Dk. Mwinyi alimuleza Waziri huyo kwamba Zanzibar ina fursa nyingi za kuekeza hasa katika Uchumi wa Buluu ambao ndio Dira ya uchumi wa Zanzibar hivi sasa.

Nae Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Sayyid Badr bin Hamad bin Hamood Al Busaid alieleza azma ya Serikali ya Oman ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kidugu uliopo baina ya pande mbili hizo.

Waziri huyo wa Mambo ya Nje alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba Serikali ya Oman iko tayari kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kukuza uchumi wake kupitia Sera yake ya Uchumi wa Buluu huku akiahidi hatua zitakazochukuliwa kuhakikisha miradi iliyosainiwa inatekelezwa kwa haraka.