Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt.Charles Mhina, amewataka Maafisa Ugani kuhakikisha wanaielewa na kwenda kuifanyia kazi teknolojia ya Uhimilishaji ili kwenda kuboresha Mifugo iliyopo kwenye maeneo yao na kuongeza tija kwa wafugaji ili waweze kufuga kibiashara.
"Lengo mama la Wizara ni kuwabadilisha wafugaji wetu waanze kufuga kibiashara lakini hilo halitawezekana kama wana ng’ombe wanaozalisha lita 2 za maziwa kwa siku badala ya lita 20 mpaka 40 kwa ng’ombe wa kisasa"Dkt.Mhina.
Dkt.Charles Mhina, ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Riziki Shemdoe, amewataka Maafisa Ugani hao kuhakikisha wanaenda kufanyia kazi kwa vitendo teknolojia zote walizofundishwa wakati wote wa Mafunzo.
Dkt.Mhina ametoa kauli hiyo Babati mkoani Manyara, na kueleza kuwa serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imehitimisha zoezi la Mafunzo Rejea kwa Maafisa Ugani 1058 waliokuwa katika kanda mbalimbali ikiwa ni lengo la kuwafikia Maafisa Ugani 1000.
Akizungumza kwa niaba ya Wakurugenzi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Babati Bi.Upendo Mangali, ameipongeza Wizara kwa kuendesha mafunzo hayo huku akitoa rai kwa Taasisi nyingine za Serikali kuiga mfano huo ili kuongeza ujuzi zaidi kwa wataalam wake.
"Watumishi wakijengewa uwezo maana yake wanajenga Imani kwa wananchi hususan wafugaji kwamba watapata huduma bora na elimu haina mwisho kila siku mambo yanabadilika kutokana na mabadiliko ya teknolojia hivyo naamini nyie ni “TOT” mtaenda kufundisha wake waliopo kwenye maeneo yenu" Amesema Bi.Mangali.
Akizungumza kwa niaba ya Maafisa Ugani wenzie Mshauri wa Mifugo wa Mkoa wa Manyara Bw.Issa Mzava, ameahidi kwenda kufanyia kazi yale yote waliyofundishwa kwenye kanda zote kwa kuzingatia kasi na weledi mkubwa.
Mafunzo Rejea hayo kwa Maafisa Ugani upande wa Sekta ya Mifugo yalifunguliwa rasmi Machi 18, 2024 Kibaha Mkoani Pwani ambapo yalifanyika kanda zote nchini kwa lengo la kuwafikia Maafisa Ugani 1000 nchi nzima.