Back to top

WAMILIKI ARDHI WASIOLIPA KODI KUCHUKULIWA HATUA

10 May 2024
Share

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Jerry Silaa, ametoa siku thelathini (30) kwa wamiliki wote wa ardhi wanaodaiwa Kodi ya Pango la Ardhi ambao hawajalipa hadi sasa kulipa kodi husika na baada ya muda huo kupita hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Waziri Silaa ameyasema hayo leo katika Ofisi za Wizara ya Ardhi zilizopo Magogoni Jijini Dar es Salaam.

Waziri Silaa amesema kuwa kila mmiliki wa ardhi analo jukumu la kulipa kodi ya pango la ardhi kila mwaka na amepewa sharti la kulipa Kodi ya Pango la Ardhi kwa kila mwaka kwa mujibu wa Fungu la 33 (1) la Sheria ya Ardhi (Sura ya 113).
 
Aidha, ameongeza kuwa kwa mujibu wa Fungu la 44 (1) la Sheria ya Ardhi (Sura ya 113), kila mmiliki wa ardhi anatakiwa kutimiza masharti ya umiliki ikiwa ni pamoja na sharti la kulipa Kodi ya Pango la Ardhi.

Silaa amesema Kitendo cha kutolipa Kodi ya Pango la Ardhi ndani ya muda uliowekwa na sheria, kinasababisha mmiliki wa ardhi kuvunja moja ya sharti la umiliki. 
 
Ameongeza kuwa Wizara kwa nyakati tofauti, imekuwa ikihamasisha na kuwakumbusha wamiliki wa ardhi kulipa Kodi ya Pago la Ardhi. Hata hivyo, baadhi ya wamiliki wa ardhi hawajatekeleza wajibu huo wa kisheria.
 
Silaa amehitimisha kwa kusema kuwa katika kipindi hicho cha siku thelathini (30), vituo vya makusanyo ambavyo ni; Ofisi za Ardhi za Mikoa na Ofisi za Ardhi za Halmashauri zote nchini, kwa siku za kazi zitakuwa wazi hadi muda wa saa 2:00 Usiku. Hivyo, naagiza watendaji wote wa Sekta ya Ardhi, kuratibu mazingira rafiki kwa ajili yakufanikisha utekelezaji wa mkakati huu.