Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Geophrey Pinda, amesema jumla ya Vijiji 45 kati ya Vijiji 61 katika Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, vimewekewa mipango ya matumizi ya ardhi.
Mhe.Pinda amesema Uvinza mji wa Uvinza kwa sasa unakuwa kwa kasi na wizara yake kupitia Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo iliamua kuviwekea Vijiji vya Wilaya ya Uvinza Mipango ya Matumizi ya Ardhi, ili kutenga maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali kama vile kilimo na ufugaji.
Mhe.Pinda ameeleza pia mgogoro baina ya wananchi wa Kijiji cha Mpeta na Ranchi ya NARCO, mgogoro uliosababishwa na wananchi wa Kijiji hicho kutoridhika na Hekta 2,500, walizopatiwa kutoka kipande cha ranchi ambapo kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi tayari serikali imesikia kilio cha wananchi hao na kuwapatia hekta nyingine 5,240 ili ziweze kutosheleza mahitaji.
Hata hivyo, amemtaka Mkuu wa wilaya ya Uvinza pamoja na mkurugenzi wa halmashauri kukaa na viongozi wengine wa wilaya hiyo kuhakikisha hekta zilizotolewa zinagawiwa kwa wananchi kwa lengo la kukidhi mahitaji.
Aidha amemulika gogoro baina ya wilaya ya Kasulu na Uvinza kuhusiana na kitalu cha uwindaji alichopatiwa mwekezaji, ambapo Mhe.Pinda amemueleza Makamu wa Rais kuwa, kitalu alichopewa muwekezaji ramani yake ina mapungufu hivyo ameielekeza ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Kigoma kukutana na halmashauri za wilaya husika husika ili kupata tafsiri sahihi ya ramani kwa lengo kutafuta suluhu ya mgogoro huo.
Makamu wa Rais Mhe. Dkt Philip Isdori Mpango yupo kwenye ziara mkoani Kigoma, ambapo mbali na mambo mengine amekagua miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile umeme na barabara.