![](https://www.itv.co.tz/sites/default/files/styles/large/public/field/image/heche.jpg?itok=PRwXNBh9)
Mbunge wa Tarime vijiji kwa tiketi ya CHADEMA John Heche amefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu Dar es Salaam na kusomewa mashitaka matatu ikiwa ni pamoja na kuunganishwa katika kesi inayowakabili viongozi 7 wa CHADEMA akiwemo mwenyekiti wa chama hicho Mhe. Freeman Mbowe.
Mhe.John Heche ameunganishwa na wenzake katika kesi hiyo ya jinai namba 112 ya 2018 na kufanya idadi ya washtakiwa kuwa 8, huku wakiwa na mashitaka 10.
Hati ya mashitaka imesomwa mbele ya hakimu mkazi mkuu, Wilbard Mashauri na wakili wa serikali mkuu Faraja Nchimbi ambapo ameieleza mahakama kuwa mshitakiwa huyo anakabiliwa na mashitaka matatu yakiwemo ya kufanya maandamano na mkusanyiko usio halali, kuendelea na mkusanyiko usio halali makosa yaliyotendeka Feb 16 mwaka huu katika barabara ya Kawawa Mkwajuni Kinondoni Dar es Salaam.
Wakili wa serikali mkuu Faraja Nchimbi ameieleza mahakama kuwa katika shtaka la tatu, 16 Feb mshtakiwa huyo akiwa katika viwanja vya Buibui wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, akihutubia katika mkutano wa hadhara alitamka maneno yenye kuchochea chuki na manung'uniko miongoni mwa jamii na wakazi wa Tanzania.