Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Biteko amesema, Ubelgiji inaunga mkono kampeni ya Nishati Safi ya kupikia na imeonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika matumizi ya nishati hiyo, kwa maendeleo ya Bara zima la Afrika, iliyoasisiwa na Kinara wa Kampeni hiyo Mhe.Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Dkt.Biteko amebainisha hayo katika Kikao na Waziri wa Nishati wa Ubelgiji, Mhe.Tinne Van Der Straeten kilichofanyika mjini Windhoek, Namibia, ikiwa ni sehemu Mkutano wa Nchi za Afika kujadili matumizi Hydrojen kutumika katika kuzalisha umeme.
Dkt.Biteko amesema ili kupata maendeleo ya kweli, Tanzania inatoa kipaumbele katika matumizi ya nishati, ambayo itawawezesha kupata maendeleo endelevu, ikiwa ni pamoja kuondokana na magojwa na vifo vinavyotokana na matumizi ya nishati isiyokuwa safi.
Amesema ushirikiano wa miaka mingi kati ya Tanzania na Ubelgiji utawezesha upatikanaji wa maendeleo yanayoweza kutokana na uwekezaji wa kimkakati kutoka kwa wafanyabiashara na wawekezaji.
"Kama mnavyofahamu, Tanzania kupitia Mhe. Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan, imeasisi na inaendeleza kampeni kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia katika kipindi cha miaka 10 ijayo kuanzia mwaka huu”amesema Dkt.Biteko na kuongeza kuwa Tanzania ingetamani kuungwa mkono na ubelgiji katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kama ambavyo imekuwa ikifafanya katika sekta nyingine ikiwemo elimu na uwezeshaji katika masuala ya usawa kijinsia.