Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, imeitaka Wizara ya Nishati kuendelea kuusimamia ipasavyo mradi wa kuzalisha umeme, katika Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) ili ukamilike kwa wakati.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Kirumbe Ng'enda wakati wa ziara ya kukagua hatua za utekelezaji wa mradi huo ambao utaingiza megawati 2,115 mara baada ya kukamilika.
"Wizara iendelee kusimamia kwa umakini mradi huu ili mashine zote Tisa ziweze kukamilika kama ilivyopangwa." Amesema Mhe. Ng'enda.
Aidha, kamati hiyo imeipongeza serikali kwa kuhakikisha mashine zilizosalia zinaendelea kukamilika na kufanya kazi, ambapo hadi sasa zimekamilika mashine tatu ambazo zinazalisha kiasi cha megawati 705 na mashine namba sita ipo kwenye hatua za mwisho kukamilishwa.
Kwa upande wake Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Wizara ya Nishati imekuwa ikifanya kazi kwa ushirikiano na kamati hiyo ya Bunge ikiwa ni pamoja na kupokea maelekezo, ushauri na mapendekezo ya Kamati.
"Kazi kubwa ya Kamati ni kutusimamia sisi Serikali, na sisi tunahakikisha kuwa maelekezo yenu yote yanatekelezwa na mafanikio yake yanaonekana katika miradi mbalimbali kama JNHPP, ambao utekelezaji wa mradi wake umefikia asilimia 98." Amesema Kapinga
Ameongeza kuwa, Wizara ya Nishati chini ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko itaendelea kuusimamia mradi huo ila ukamilike kwa wakati.
Ameeleza kuwa, Mkandarasi wa mradi ameshalipwa takriba shilingi trilioni 6.3 kati ya shilingi trillioni 6.5 zinazopaswa kulipwa.