Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata kilogramu 1,815 za dawa za kulevya aina ya skanka katika operesheni iliyofanyika tarehe 28 Agosti, 2024 hadi tarehe 02 Septemba, 2024 katika maeneo ya Luguruni Mbezi na Magomeni jijini Dar es Salaam ambapo watuhumiwa watano (05) wamekamtwa kuhusiana na dawa hizo.
Watuhumiwa waliokamatwa wanatambulika kwa majina ya Richard Henry Mwanri (47) ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi Makonde wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na Felista Henry Mwanri (70) mkulima na mkazi wa Luguluni Mbezi wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam ambaye ni mmiliki wa nyumba zilipokutwa dawa hizo za kulevya.
Watuhumiwa wengine ni Athumani Koja Mohamed (58) mfanyabiashara, na mkazi wa Tanga, Omary Chande Mohamed (32) dereva bajaji na mkazi wa Buza jijini Dar es Salaam na Juma Abdallah Chapa (36) mkazi wa Kiwalani jijini Dar es Salaam. Aidha, katika operesheni hiyo, gari aina ya Mitsubishi Pajero yenye namba za usajili T 551 CAB na bajaji yenye namba za usajili MC 844 CZV vilikamatwa.
Richard Mwanri ni mhalifu ambaye amekuwa akipokea dawa za kulevya kutoka nchi mbalimbali na kuziingiza nchini kwa usafiri wa magari zikiwa zimefichwa kwa kuchanganywa na bidhaa nyingine kisha kusambazwa kwa wauzaji wengine katika maeneo mbalimbali nchini. Kwa siku za hivi karibuni, dawa za kulevya aina ya skanka zimekuwa zikikamatwa mara kwa mara nchini. Skanka ni aina ya bangi ya kusindika yenye kiwango kikubwa cha kemikali yenye sumu aina ya Tetrahydrocannabinol (THC) ambayo inaweza kuharibu mfumo wa fahamu, akili na kusababisha magonjwa yasiyoambukiza kama vile moyo, figo, na ini. Matumizi ya skanka kwa wajawazito yanaweza kusababisha madhara kwa mtoto aliye tumboni ikiwemo kuathiri maendeleo ya ubongo na kuzaliwa na uzito mdogo.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya ya Dunia iliyotolewa Vienna nchini Austria tarehe 26 Juni, 2024, maeneo yaliyohalalisha matumizi ya bangi, uzalishaji wa bidhaa za bangi zenye kiwango kikubwa cha kemikali ya THC uliongezeka. Aidha, taarifa hiyo inaeleza kuwa, katika nchi hizo, kumekuwa na ongezeko la watu wanaohitaji tiba kutokana na matumizi ya bangi sambamba na kuongezeka kwa watu wenye matatizo ya akili na waliojaribu kujiua.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inawasihi wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara hii haramu na kuhamasishana kutoshiriki katika biashara wala matumizi ya dawa za kulevya.
Aidha, watumishi wanaofanya kazi katika vituo vya forodha vya mipakani hususani wanaohusika na ukaguzi wa magari na bidhaa zinazoingia na kutoka nchini, waendelee kuwa makini wanapotekeleza majukumu yao kwani wahalifu wa dawa za kulevya hubuni mbinu za kuficha ili kusafirisha dawa za kulevya.
Ukamataji mkubwa wa dawa za kulevya unaofanyika nchini ni matokeo chanya ya uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali ya awamu ya sita, chini ya uongozi thabiti wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amedhihirisha dhamira ya kulinda kizazi cha sasa na kijacho kwa kuimarisha mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya.
Pia, ni matunda ya elimu ya dawa za kulevya inayoendelea kutolewa nchini ambayo imehamasisha wananchi kuwa na mwamko wa kutoa taarifa dhidi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
Mmlaka itaendelea kuwa macho na kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya wote wanaoharibu nguvu kazi ya taifa kwa kujihusisha na dawa za kulevya kwa namna yoyote ile.