Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ametumia jukwaa la Mkutano wa 8 wa Mawaziri wa Uvuvi wa Bahari na Maji ya Ndani kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Karibiani na Pasifiki kuainisha fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye Sekta ya Uvuvi nchini.
Mhe. Majaliwa amenadi fursa hizo wakati wa hotuba yake ya Ufunguzi wa Mkutano huo aliyoisoma kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo amesema kuwa Tanzania ina rasilimali kubwa za maji ikiwa ni pamoja na bahari ya Hindi, maziwa, mito,mabwawa ya asili na ya kutengenezwa.
"Pia tuna ardhi yenye rutuba, hali nzuri ya hewa na mfumo wa kisheria unaohamasisha maendeleo ya kilimo cha samaki ambapo mpaka sasa tumezalisha tani 43411 ikiwa ni sawa na asilimia 9 ya uzalishaji wote wa samaki hapa nchini" Amesema Mhe. Majaliwa.
Aidha Mhe. Majaliwa amesema kuwa Tanzania ina eneo kubwa la kiuchumi lenye ukubwa wa kilomita za mraba 223,000 ambalo ni takribani ya asilimia 24 ya ardhi yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo amebainisha kuwa uvuvi unaofanywa hivi sasa kwenye eneo hilo ni ule wa mataifa ya uvuvi ya maji ya mbali.
"Hivyo eneo hilo ni fursa kubwa kwa yoyote mwenye nia ya kuwekeza hapa nchini ambapo anaweza kufanya hivyo kupitia uwekezaji wa ununuzi wa meli za uvuvi na huduma zake, usambazaji wa zana za Uvuvi, chakula cha samaki na eneo lolote ambalo mnadhani litawavutia kuwekeza kwenye sekta ya Uvuvi nchini" Amesisitiza Mhe. Majaliwa.
Akiwasilisha taarifa ya utangulizi kuhusu yale yatakayojadiliwa kwenye mkutano huo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema yeye na mawaziri wenzake wanaoshughulikia sekta ya Uvuvi watatumia jukwaa hilo kujadiliana na kukubaliana kuhusu mikakati ya kuhakikisha Uvuvi mdogo unaboreshwa kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wavuvi hao.
"Maeneo yatakayojadiliwa ili kuboreshwa kwa ajili ya wavuvi hao ni pamoja na upatikanaji wa mitaji, teknokojia za kisasa, masoko na miundombinu" Amesema Mhe. Ulega.
Aidha Mhe. Ulega ameongeza kuwa mkutano huo utaangazia changamoto zinazotishia ustawi wa rasilimali za bahari na Uvuvi ikiwa ni pamoja na athari za mabadiliko ya tabia nchi na uvunaji uliopitiliza.
Mkutano huo wa 8 wa Mawaziri wa Uvuvi wa Bahari na Maji ya Ndani kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Karibiani na Pasifiki ulitanguliwa na mkutano wa Wataalam wa nchi hizo uliofanyika Septemba 09, 2024.